Chimbuko

Chimbuko

CHIMBUKO LA KITUO CHA URITHI WA UKOMBOZI WA BARA LA AFRIKA

Chimbuko la Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika linatokana na jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuhakikisha historia, mchango na urithi wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika vinatambuliwa, vinahifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mwaka 2003, Tanzania ilifanya tathmini kwa kushirikiana na wadau wa urithi wa ukombozi wa Afrika. Tathmini hiyo ilibaini kuwa, licha ya Tanzania kuwa kitovu cha harakati za ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, kulikuwa na upungufu mkubwa wa utambuzi, uhifadhi na uendelezaji wa vielelezo vinavyoonesha historia hiyo muhimu. Kutokana na hali hiyo, wadau wa urithi, wakiongozwa na UNESCO, walipendekeza kuanzishwa kwa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika ili kuratibu utambuzi, uhifadhi na uendelezaji wa urithi huo. Serikali ya Tanzania ilikubali na kuanza kuratibu utekelezaji wa wazo hilo.

Mwaka 2004, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNESCO ilifanya ziara za mashauriano katika nchi za Angola, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe. Mashauriano hayo yalikubaliana kuwa Programu ihusishe nchi zote za Kusini mwa Afrika na uratibu wake ufanywe na Tanzania.

Mwaka 2005, Tanzania iliwasilisha rasmi pendekezo la Programu katika Mkutano Mkuu wa 33 wa UNESCO, ambapo liliungwa mkono na nchi 11 za Afrika, ambazo ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe. UNESCO iliridhia Programu hiyo na kuiingiza katika Mpango Mkakati wake wa kipindi cha mwaka 2008–2012.

Baadaye, mikutano mbalimbali ya kimataifa iliendelea kuimarisha wazo hilo, ikiwemo Mkutano wa Kimataifa wa Mashauriano uliofanyika Windhoek, Namibia (2008), Mkutano wa Mawaziri wa Utamaduni wa Umoja wa Afrika uliofanyika Algiers, Algeria (2008), na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Viongozi wa Vyama vya Ukombozi uliofanyika Dar es Salaam mwaka 2010. Mikutano hiyo ilisisitiza kuwa Programu hiyo ipanuliwe ili ihusishe nchi zote za Bara la Afrika.

Kutokana na mafanikio ya hatua hizo, mwaka 2011, Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ulipitisha uamuzi Assembly/AU/Dec.357(XVI) ulioridhia utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika na kuamua kuwa Makao Makuu yake yawe Dar es Salaam, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uamuzi huo uliiwezesha Tanzania kuanzisha Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kama taasisi yenye jukumu la kuratibu utambuzi, uhifadhi, utafiti, ukusanyaji wa nyaraka na vielelezo, uendelezaji na utangazaji wa urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika kwa niaba ya Umoja wa Afrika.

Hivyo, Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kilianzishwa ili kuhifadhi na kuendeleza urithi unaotokana na harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, ikiwemo picha, filamu, simulizi za mashahidi, nyaraka, barua, hotuba za viongozi, machapisho, ramani, nyimbo, sare, zana mbalimbali, mahandaki, makaburi, makambi ya wapigania uhuru na maeneo mengine ya kihistoria yanayoshuhudia mchango wa Waafrika katika kupigania uhuru wa bara lao. Kupitia Kituo hiki, urithi huo unatambuliwa, unahifadhiwa, unafanyiwa utafiti, unatumiwa kwa elimu na utalii, na kurithishwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

lbl_need_any_help