Ujumbe wa viongozi na wataalamu kutoka taasisi bin...

Ujumbe wa viongozi na wataalamu kutoka taasisi binafsi na serikali ya Jamhuri ya Msumbiji umetembelea Makavazi ya Kituo cha Urithi wa Ukombozi

16 Julai, 2026
Ujumbe wa viongozi na wataalamu kutoka taasisi binafsi na serikali ya Jamhuri ya Msumbiji umetembelea Makavazi ya Kituo cha Urithi wa Ukombozi


Viongozi na wataalamu kutoka taasisi binafsi na serikali ya Jamhuri ya Msumbiji wamefanya ziara ya kutembelea makavazi ya Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kwa lengo la kuona namna urithi wa historia ya ukombozi wa Afrika inavyohifadhiwa na kurithishwa katika jamii.

Ujumbe huo umeongozwa na mwanahistoria Bw. Fernando Dava aliyeambatana na Mkurugenzi wa Urithi wa Utamaduni wa Msumbiji, Bw. Celio Tiane, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Viwanda, Bw. Ericson Dos Santos, Maafisa waandamizi wa Ubalozi wa Msumbiji nchini pamoja na wataalamu wa masuala ya utamaduni kutoka Jamhuri ya Msumbiji.

Ujumbe huo umepokelewa na kupewa maelezo pamoja na kupitishwa katika makavazi ya Kituo yaliyosheheni kumbukumbu za historia ya ukombozi wa Afrika ikiwemo nchi ya Msumbiji.

Bw. Fernando Dava ambae ni Mkuu wa ujumbe huo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara yenye dhamana na Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kwa jitihada za kuendelea kuhifadhi kumbukumbu za urithi wa ukombozi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, Bw. Dava ameongeza kwa kusema, Msumbiji na Tanzania zitaendelea kushirikiana katika kuimarisha uhusiano wa kindugu na kihistoria kwa kuenzi kwa pamoja urithi huu ulioachwa na waasisi wa mataifa haya mawili.

lbl_need_any_help