Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kimeungana na Jamhuri ya Cuba kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa kiongozi wa Mapinduzi ya Cuba, Fidel Castro Ruz, kupitia maonesho maalum ya picha na michoro yaliyoandaliwa ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango na heshima ya maisha na uongozi wake.
Maonesho hayo yamefanyika Agosti 12, 2026 katika Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere, Magomeni Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, wanadiplomasia, viongozi, wananchi na wadau mbalimbali kutoka Tanzania na Cuba.
Katika historia itakumbukwa kuwa, Fidel Castro ni mmoja wa viongozi wa kimataifa waliotoa mchango wa kisiasa, kijeshi na kidiplomasia katika kuunga mkono mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi barani Afrika.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera, amesema Cuba itaendelea kuthamini urafiki na historia inayounganisha mataifa haya mawili, hususan katika kuenzi kumbukumbu ya Fidel Castro na Mwalimu Julius Nyerere.
Tanzania na Cuba zinaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kihistoria kwa kuendelea kushirikiana katika nyanja za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kielimu ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuenzi falsafa za waasisi wa mataifa haya mawili.