Habari
MAAFISA UTAMADUNI MMEBEBA DHAMANA YA KUSIMAMIA UTAMADUNI WA NCHI
MAAFISA UTAMADUNI MMEBEBA DHAMANA YA KUSIMAMIA UTAMADUNI WA NCHI
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka Maafisa Utamaduni nchini washiriki na kusimamia vyema shughuli za Utamaduni katika maeneo yao pamoja na kulinda mila na desturi za Kitanzania.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa maelekezo hayo Aprili 14, 2023 Wilayani Bagamoyo wakati akifungua mafunzo elekekezi kwa Maafisa Utamaduni wa Wilaya za Zanzibar ambapo ameeleza kuwa, mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Maafisa hao ikiwemo kusimamia vyema suala la Maadili, Urithi wa Utamaduni, na Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika.
"Serikali zote mbili zinatambua umuhimu wa mfunzo haya Kwa sababu Maafisa Utamaduni mmebeba dhamana kubwa ya nchi ikiwemo kukuza na kuendelea lugha yetu ya Kiswahili, kuendeleza Sekta za Sanaa na Ubunifu pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wadau wetu" amesema Mhe. Pindi Chana
Awali Kamisha wa Utamaduni wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Omar Mohamed amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kubadilishana uzoefu katika Sekta ya Utamaduni na Sanaa ili kuwa na maendeleo ya pamoja.
Mafunzo hayo yamebeba mada tofauti ikiwemo ya majukumu ya Maafisa Utamaduni ya Kisera na Kimuundo, Uhifadhi na Uendelezaji wa Urithi wa Utamaduni pamoja na Uhifadhi na Uendelezaji wa Urithi wa Bara la Afrika.