Dar es Salaam, Septemba 15, 2026
Bi Minael Mdundo, mwandishi na shahidi wa matukio ya kihistoria ya harakati za ukombozi wa Afrika, amekutana na wanafunzi wanaofanya mafunzo ya vitendo katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika na kuwashirikisha ushuhuda wa matukio mbalimbali katika kipindi cha harakati za ukombozi wa bara la Afrika.
Katika mazungumzo hayo, Mama Mdundo ameeleza nafasi ya Dar es Salaam kama kitovu muhimu cha harakati za ukombozi, akirejea mkutano wa mwaka 1962 uliofanyika katika ukumbi wa Anatoglu, Mnazi Mmoja, uliolenga kuunganisha MANU, UNAMI na UDENAMO katika harakati za kudai uhuru wa Msumbiji chini ya uongozi wa Eduardo Mondlane.
Pia ametoa ushuhuda kuhusu mwanzo wa mapambano ya silaha nchini Msumbiji mwaka 1964, pamoja na kumbukumbu za namna wapigania uhuru kutoka vyama vya kusini mwa Afrika walivyokuwa wanakutana katika maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam hususani mgahawa wa Zahir walipokuwa wakila chakula.
Ushuhuda huu ni sehemu ya historia hai ya ukombozi wa Afrika, unaowapa wanafunzi fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwa mashahidi wa matukio hayo, huku ukiendeleza juhudi za Kituo za kukusanya na kuhifadhi historia kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.