Kambi ya Itumbi | Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya
Kambi ya Itumbi ni moja ya maeneo muhimu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika yaliyopo chini ya Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika. Kambi hii ilianzishwa mwaka 1965 katika Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, na ilitumika kama kituo cha mapokezi, makazi, mafunzo na uratibu wa shughuli za wapigania uhuru kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika.
Kambi hii ilitumiwa na wapigania uhuru wa vyama vya PAC (Pan Africanist Congress) na ANC kutoka Afrika Kusini, MPLA kutoka Angola, pamoja na wapigania uhuru kutoka Zimbabwe na kwa kipindi kifupi wapigania uhuru wa FRELIMO kutoka Msumbiji. Ndani ya kambi hiyo kulikuwepo mabweni, zahanati, ghala, eneo la gwaride na shughuli za mafunzo, pamoja na miundombinu ya kuwahudumia wapigania uhuru waliokuwa wakijiandaa kwa mapambano ya ukombozi.
Leo hii, Kambi ya Itumbi ni ushahidi wa mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika. Eneo hili linaendelea kuhifadhiwa kama sehemu ya urithi wa kihistoria ili kuenzi mshikamano wa Waafrika, kujifunza historia ya ukombozi, na kuhamasisha vizazi vya sasa na vijavyo kuthamini amani, uhuru na umoja wa bara la Afrika.
Kambi ya Itumbi ni mojawapo ya maeneo yaliyokaliwa na wapigania uhuru wa vyama vya PAC, ANC na ZAPU.
Kambi ipo katika:-
Kitongoji cha Itumbi
Kijiji cha Matundasi
Kata ya Makongorosi
Tarafa ya Kiwanja
Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya